Je, Mungu anajali unavyovaa na kujipamba?

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Baadhi ya watu hudhani kuwa namna mtu anavyoonekana kwa watu wengine si muhimu ili mradi tu ndani ya moyo wake yuko safi wakidai kuwa Mungu haangalii nje bali anaangalia ndani ya moyo tu. Je, ni kweli Mungu anaangalia muonekano wa ndani pekee na hajali kabisa mwonekano wa nje?

Ni kweli Mungu haangalii kama wanadamu wanavyoangalia (1 Samueli 16:7) lakini hii haimanishi kwamba hajali mwonekano wetu wa nje. Mwonekano wa nje ni muhimu sana kwa Mungu kwa kuwa unadhihirisha utukufu na uwezo wake wa uumbaji. Mungu alituumba kwa mfano wake (Mwanzo 1:27), kabla hajatuumba katika tumbo alitujua (Yeremia 1:5) na sisi ni kazi yake (Waefeso 2:10). Mungu alituumba ili tuonekane kama alivyotaka yeye kwa kuakisi uzuri wake Yeye wenyewe. Biblia haisemi ni kwa namna gani tutaakisi uzuri wa Mungu lakini ni dhahiri kwamba mwonekano wetu unapaswa kuendana na uzuri aliokusudia.

Mojawapo ya utambulisho muhimu wa mtu ni namna anavyoonekana hasa katika mavazi, mapambo na vipodozi. Unaweza kujua kazi ya mtu kwa kuangalia mavazi yake. Kwa mfano, unaweza kumjua mtu kama ni askari, daktari, muuguzi, mwanafunzi na kadhalika kupitia mavazi yake tu.

Unaweza pia kutambua dini ya mtu kwa kuangalia tu mavazi yake. Kwa mfano, ukikutana na mwanamke aliyevaa hijabu, au mwanaume aliyevaa kanzu na baraghashia mtu huyo anaweza kuwa ni mwislamu. Ukikutana na mwanaume aliyevaa kola shingoni, ni wazi kuwa huyo atakuwa mchungaji wa baadhi ya makanisa ya kikristo. Mwonekano pia unaweza kutambulisha kabila au taifa la mtu. Kwa mfano, ukikutana na mtu amevaa lubega, bila shaka huyo atakuwa ni mtu anayetoka katika kabila la wamasai.

Zaidi ya utambulisho wa kazi, dini, kabila na kadhalika, mwonekano wa mtu unatambulisha tabia ya mtu pia. Kwa mfano, kwa kuangalia mwonekano wake wa nje kupitia mavazi na nywele, unaweza kumjua mtu mwenye tabia ya usafi au uchafu. Vilevile, unaweza kumtambua mtu mwenye adabu au heshima kwa kuangalia mavazi yake kwa mtazamo wa jamii anayotoka.

Katika kila jamii, kuna mavazi ambayo mtu akiyavaa atatafsiriwa kuwa ana adabu au vingivevyo. Kwa hiyo, suala la mavazi, mapambo na vipodozi ni muhimu sana maana hutufanya tuwe na mwonekano fulani ambao unaweza kututambulisha kama kweli sisi ni wakristo au la. Vilevile, mwonekano wa nje unaweza kututambulisha maadili yetu kama tuna maadili mema au mabaya.

Kuna kisa cha mtu mmoja ambaye aliamua kusimama kando ya lango kuu la kuingilia katika kanisa fulani siku ya ibada. Mtu huyo alikuwa amevaa nguo pana, chafu na zilizochanika na yeye mwenyewe akiwa mchafu na hakuwa amechana nywele. Waumini walipokuwa wakipita kuelekea kanisani, hakuna aliyesimama na kumsalimia mtu huyo. Wiki iliyofuata, mtu huyo alitambulishwa kuwa ndiye mchungaji mpya wa kanisa hilo. Baada ya kutambulishwa, mchungaji huyo aliwaeleza waumini wake kuwa alifanya hivyo ili kuwafundisha kwa vitendo somo la kutopendelea watu kwa kutazama mwonekano wao wa nje (Yakobo 2:2-9).

Biblia katika Yakobo 2:2-9 inasema “Ndugu zangu, imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe nayo kwa kupendelea watu. 2 Maana akiingia katika sinagogi lenu mtu mwenye pete ya dhahabu na mavazi mazuri; kisha akiingia na maskini, mwenye mavazi mabovu; 3 nanyi mkimstahi yule aliyevaa mavazi mazuri, na kumwambia, Keti wewe hapa mahali pazuri; na kumwambia yule maskini, Simama wewe pale, au keti miguuni pangu, 4 je! Hamkufanya hitilafu mioyoni mwenu, mkawa waamuzi wenye mawazo mabovu? 5 Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao? 6 Bali ninyi mmemvunjia heshima maskini. Je! Matajiri hawawaonei ninyi na kuwavuta mbele ya viti vya hukumu? 7 Hawalitukani jina lile zuri mliloitwa? 8 Lakini mkiitimiza ile sheria ya kifalme kama ilivyoandikwa, Mpende jirani yako kama nafsi yako, mwatenda vema. 9 Bali mkiwapendelea watu, mwafanya dhambi na kuhukumiwa na sheria kuwa wakosaji”.

Kisa hiki kinaonesha wazi kuwa mwonekano wa nje wa mtu una nafasi yake katika kuhitimisha juu ya mambo kadhaa kuhusu mtu huyo. Kwa kuwa mtu yule alikuwa ni mchungaji, waumini wake walitegemea angevaa mavazi yenye hadhi ya kichungaji. Kwa kuvaa mavazi yenye hadhi isiyo yake, waumini wake walimpatia hadhi isiyo yake pia.  Ukiacha dhambi ya ubaguzi ambayo waumini hao walitenda,  kisa hiki kinadhihirisha kuwa mwonekano wa nje wa mtu unaweza kusababisha atendewe kitu fulani kwa ubaya au uzuri.

Ni wazi kwamba mwonekano wa mtu unaweza kuathiri mtazamo wetu juu ya mtu huyo na vilevile mwonekano wetu wa nje unaweza kuathiri mtazamoa wa watu wengine kuhusu sisi. Kwa sababu hiyo, tunapaswa kuwa makini sana kuhusu tunavyoonekana ili watu wanaotuangalia wasiwe na mtazamo tofauti na jinsi tulivyo. Mtazamo usio sahihi kuhusu sisi unaweza kuwa na athari hasi katika maisha yetu kama wakristo. Kwa mfano, ukienda katika jamii inayoamini kuwa wanawake wanaovaa suruali ni malaya, basi jamii itakutambua kuwa wewe ni malaya hata kama kwa uhalisia wewe si malaya. Mtazamo huu usio sahihi unaweza kuathiri hata upelekaji wa injili kwa watu hao. Watu hawawezi kukusikiliza kama utawahubiria habari za Yesu kwa kuwa wanaamini wewe ni malaya na hivyo haufuati maadili ya kikristo. Kama wewe hufuati maadili ya kikristo utawaambiaje wao wawe wakristo na waishi maisha ya kirsto ambayo wewe unayavunja?

Mwonekano wa nje usioleta utukufu kwa Mungu ni ishara inayoonesha tatizo la kiroho. Kwa mtu yeyote mwenye akili timamu, anapoamua kuvaa aina fulani ya nguo, kunyoa mtindo fulani wa nywele, kutumia mapambo na vipodozi vya aina fulani hufanya hivyo kwa uchaguzi wake mwenyewe. Kinachomsukuma kufanya uchaguzi huo ni kile kilicho ndani ya moyo wake. Kama ndani ya moyo wake anaona kitu au kitendo hicho kiko sawa atafanya na kama anaona hakiko sawa hawezi kufanya.

Hivyo, mwonekano wa nje ni kiashiria cha wazi cha kile kilicho ndani ya moyo wa mtu. Kwa mfano, mtu ambaye si kahaba ndani ya moyo wake, hawezi kuvaa mavazi ya kikahaba. Japo wakati mwingine, mtu mnafiki anaweza akawa na mwonekano wa nje ambao ni tofauti na alivyo ndani ya moyo, lakini kwa hali ya kawaida, huwezi ukatenganisha kilicho ndani ya moyo wa mtu na mwonekano wake wa nje. Ukristo ulio ndani ya moyo hauwezi kubaki ndani ya moyo tu bali utaonekana kwa nje pia. Hivyo, mwonekano wa nje ni kiashiria cha ukristo wenu.

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mavazi, mapambo na vipodozi?

Basi tafuta kitabu chetu kinachoitwa Mwonekano wa Mkristo: Kanuni Zinazokubalika Kibiblia, Kiafya na Kijamii Kuhusu Mavazi, Mapambo na Vipodozi. Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na Email:  spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mapngo wa Mungu kuhusu mafanikio yako?

Basi jiunge na mtandao wa www.mkristomafanikio.co.tz. Mtandao huu umeanzishwa kwa kusudi la kuwapatia maarifa ya msingi katika nyanja mbalimbali za maisha. Katika mtandao huu utapata maarifa katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano, malezi ya watoto na mambo mengine ya kiroho.

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

1 comment / Add your comment below

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *