Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Suala la mavazi yanayomfaa mkristo ni mojawapo ya masuala tete katika ulimwenguni wa leo wenye mwingiliano wa tamaduni mbalimbali unaosabishwa na utandawazi. Kwa miaka ya nyumba hakukuwa na kelele nyingi sana kuhusu suala hili maana watu wengi walikuwa wanavaa mavazi ya kujisitiri. Kutokana na mwingiliano wa tamaduni mbalimbali, watu wanaiga mavazi kutoka katika tamaduni zingine na kusababisha baadhi ya watu kutoyakubali baadhi ya mavazi na kuyaona kama siyo ya kujisitiri.
Wahanga wakubwa wa tatizo la mavazi ya kujisitiri ni wanawake hasa wasichana. Hao ndio wanavaa mitindo mbalimbali ya mavazi yanayolalamikiwa na jamii kuliko wanaume. Baadhi ya mavazi yanayolalamikiwa ni pamoja na sketi fupi maarufu kama mini-skirt, suruali na kaptura za kubana, magauni mafupi, blauzi zinazoacha baadhi ya sehemu za mwili zikiwa wazi kama kama vile tumbo.
Mavazi ya kujisitiri ni yapi?
Pengine swali la kujiuliza ni hili, mavazi ya kujisiriti ni yapi?
Kwa bahati mbaya, hakuna sheria yoyote hapa nchini Tanzania inayofafanua kuwa mwanamke wa kitanzania anapaswa avaaje. Hata hivyo, upo mwongozo wa mavazi kwa watumishi wa umma lakini wasio watumishi wa umma hauwahusu. Hali hii inawafanya watu wengi washindwe kuelewa mavazi yakujisitiri ni yapi na yasiyo ya kujisitiri ni yapi. Pamoja na kukosekan kwa sheria au mwongozo kuhusu mavazi kwa watanzania, wakristo hawana sababu ya kuchanganyikiwa kwa kuwa Biblia imeweka mwongoz ulo wazi kabisa kuhsu suala hili.
Miaka mingi iliyopita. Kulikuwa na changamoto kama tuliyo nayo leo kwa wakristo kuvaa mavazi yasiyompendeza Mungu. Hali hii ilipelekea Mtume Paulo kuandika Waraka kwa wakristo wa wakati huo kupitia kwa Timotheo. Katika waraka huo, Mtume Paulo alielekeza yafuatayo “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi” (1 Timotheo 2:9a).
Japo mazingira yetu na ya wakati ule waraka unaandikwa yako tofauti , lakini maelekezo haya ni kanuni isyopitwa na wakati na hiyo ndiyo inapaswa kuwaongoza wakristo kujua mavazi ya kujisitiri ni yapi. Kanuni hii inajibu swali letu kuhusu mavazi ya kujisitiri ya yapi.
Ili kuelewa mavazi ya kujisitiri ni yapi, ni vizuri kwanza kuelewa maana ya neno kujisitiri. Neno kujisitiri linatokana na neno sitiri. Kwa mujibu wa Kamusi Teule ya Kiswahili neno sitiri maana yake ni “kuficha kitu ama jambo la aibu ili lisionekane; ficha soni; funika”. Kutokana na maana hii ya neno kujisitiri, ni wazi kwamba mavazi ya kujisitiri ni mavazi ambayo yanafunika sehemu za mwili ambazo zikionekana zinaleta aibu kwa mtu. Kwa muktadha wa tamaduni nyingi za kitanzania na kiafrika kwa ujumla, kuna sehemu za mwanamke ambazo kwa kawaida zinapaswa kufunikwa kama vile mapaja, tumbo, matiti, makalio na sehemu za siri. Hivyo, mavazi yoyote ambayo yatasababisha sehemu hizi zionekane, basi mavazi hayo si mavazi ya kujisitiri na kwa sababu hiyo hayafai kuvaliwa na mwanamke.
Kwa mujibu wa kitabu cha ufafanuzi wa Biblia kiitwacho John Gill’s Exposition on the Entire Bible, neno lililotafsiriwa kama mavazi katika 1 Timotheo 2: 9 linamaanisha vazi refu linalofika chini miguuni na neno lililotafsiriwa –“a kujisitiri” linamaanisha safi, maridadi, nzuri, ya heshima, ya kuvutia. Hivyo, Paulo katika 1 Timotheo 2:9 alimaanisha kwamba miili ya wanawake inapaswa kufunikwa kwa nguo safi na za heshima.
Mwanamke mkristo anapaswa kufahamu kuwa uzuri wa mwanamke hautokani na kile tu anachokionesha kama vile mavazi mazuri na mapambo bali unatokana pia na kile anachokisitiri. Mwanamke anayevaa ili kuonesha sehemu za mwili ambazo kwa kawaida anapaswa kuzisitiri anawafanya wanaume wamuone kama kifaa cha kujistarehesha kwa njia ya ngono. Kwa kufanya hivyo, uzuri na thamani yake kama mwanamke vinapungua. Ili kulinda uzuri na thamani yake, mwanamke anapaswa kujipamba kwa mavazi ya kujisitiri.
Uzuri na uthamani wa mwanamke unaweza kufananishwa na madini. Kuna madini yanayopatikana kirahisi katika uso wa ardhi au katika kina kifupi cha ardhi na yale yanayopatikana katika kina kirefu ndani ya ardhi. Mifano ya madini yanayopatikana juu ya ardhi ni mchanga, mawe na changarawe. Madini yanayopatikana ndani ya ardhi ni kama vile dhahabu, almasi, shaba, tanzanite, lulu na fedha.
Madini yanayopatikana ndani ya ardhi kwa kawaida yana thamani kubwa kuliko yale yanayopatikana juu ya uso wa ardhi au katika kina kifupi cha ardhi. Ili kupata madini yaliyo chini ya ardhi, lazima utumie jitihada kubwa kuyapata lakini madini yaliyo juu ya ardhi unaweza kuyapata bila jitihada kubwa.
Mwanamke anayevaa mavazi ya kujisitiri ni sawa na madini yanayopatikana chini ya ardhi. Kutokana na uthamni wake si rahisi kumpata mwanamke huyu kwa ajili ya kujistarehesha kingono. Lakini, mwanamke anayevaa mavazi yasiyo ya kujisiti anafananishwa na madini yaliyo juu ya ardhi. Moja ya makusudi ya kuvaa nguo zisizo za kujisitiri ni kuvuta watu ili wamtamani kwa ajili ya kufanya naye ngono. Kwa sababu hiyo, anaweza kupatikana kirahisi kwa ajili ya kutumiwa na wanaume kujistarehesha kiongono. Ndiyo maana wanawake wanaofanya biashara ya kujiuza miili, maarufu kama machangudoa, huwa wanavaa mavazi yasiyo ya kujisitiri.
Kwa hiyo, kuvaa nguo za kujisitiri ni kujipandisha thamani na heshima yako yako lakini kuvaa nguo zisizo za kujisitiri ni kujishusha thamani na heshima yako wewe mwenyewe katika jamii. Sasa, uchaguzi ni wetu, ama kuwa watu wa thamani au kujishusha thamani yetu mbele ya watu wengine.
Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mavazi, mapambo na vipodozi?
Basi jipatie kitabu chetu kinachoitwa Mwonekano wa Mkristo: Kanuni Zinazokubalika Kibiblia, Kiafya na Kijamii Kuhusu Mavazi, Mapambo na Vipodozi. Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na Email: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.
Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mapngo wa Mungu kuhusu mafanikio yako?
Basi jiunge na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio. Mtandao huu umeanzishwa kwa kusudi la kuwapatia maarifa ya msingi katika nyanja mbalimbali za maisha. Katika mtandao huu utapata maarifa katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano, malezi ya watoto na mambo mengine ya kiroho.