Je, Unataka Kujua kwa nini Wanawake Hupenda Kuvaa ‘Vimini’? Soma hapa

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Mojawapo ya mambo ambayo Mungu wetu anayajali sana na ameyatolea maelekezo bainifu ni mwonekano wetu wa nje hususani katika mavazi, mapambo na vipodozi. Kwa mfano, kupitia katika 1 Timotheo 2:9-10 na Petro 3:1- 5, Mungu anasisitiza juu ya wakristo kuvaa mavazi ya heshima, yaani mavazi ya kujisitiri na yenye adabu.

Tamaduni nyingi hasa za Kiafrika, zinakubaliana na fundisho hili la kuvaa nguo za heshima. Katika tamaduni hizo, nguo za heshima kwa wanawake ni zile zinazofunika sehemu kubwa ya mwili na kubakiza sehemu chache tu kama vile kichwa, mikono na miguu chini ya magoti.

Mtu yeyote anayevaa nguo zinazoonesha sehemu kubwa ya mwili wake au zinazobana kiasi cha kumfanya maungo yake yaonekane, huyo anahesabika amevaa nguo zisizo za heshima.

Mfano mzuri wa nguo isiyo ya heshima ni sketi fupi maarufu kama vimini au mini-skirt. Hizi ni sketi ambazo urefu wake uko juu ya magoti na kwa kawaida huwa ni za kubana. Mtu anayevaa sketi hizi huwa anaacha wazi mapaja yake na asipokuwa makini anapokaa anaweza kuonesha nguo zake za ndani. Kwa vigezo vyovyote, hii si nguo  ya heshima.

Kwa kawaida mavazi yasiyo ya heshima kama mini-skirt yanasababisha watu wengi wamfikirie vibaya mvaaji. Jinsi tunavyovaa huongoza maoni ya wale tunaokutana nao katika maisha ya kila siku juu ya hali zetu za ndani na mtindo wa maisha tuliouchagua.

Wavulana na wanaume wengi wenye tamaa ya ngono wanapomwona mwanamke aliyevaa mavazi yanayoonesha sehemu za mwili ambazo kwa kawaida huwa haziachwi wazi wanatambua kuwa wanakaribishwa na mwanamke huyo kwa ajili ya kupata starehe ya ngono. Hii ni kwa sababu wanaume na wanawake wana utofauti juu ya namna wanavyovutiwa kufanya ngono.

Kwa kawaida, wanaume huvutiwa na wanawake kwa kutazama lakini wanawake huvutiwa na wanaume kwa kuguswa. Hivyo, ni rahisi sana mwanaume kupata ashiki ya kufanya ngono anapomuona mwanamke ameacha wazi maungo yake ya mwili au amevaa nguo ya kubana inavyoonesha namna umbo lake lilivyo.

Mavazi mafupi sana yanayoacha mapaja wazi hayafai kwa mwanamke mkristo anayejiheshimu kwa sababu yanawafanya wanaume watamani kufanya naye ngono. Si hivyo tu, bali pia mavazi hayo yanawafanya watu wamfikirie kuwa ana tabia ya kikahaba na hivyo heshima yake inashuka mbele ya jamii.

Mwanamke anayejiheshimu hawezi kuvaa mini-skirt kama hana lengo la kuwavutia wanaume wafanye naye ngono. Hata wanawake wanaojiuza miili yao kwa ajili ya ngono maarufu kama machangudoa mara nyingi huvaa mini-skirt. Hivyo, ni kitu cha ajabu mtu mwingine ambaye si changudoa kuvaa mini-skirt. Anavaa nguo hiyo ili iweje? Mwanamke yeyote anayevaa na kujipamba kwa lengo la kuwavutia wanaume ni dhahiri kuwa anajidhalilisha na kujishushia heshima yake. Anajiweka katika mazingira ambayo wanaume watamwona kama chombo cha kujistarehesha tu.

Nani alibuni mini skirts na kwa nini?

Mini-skirts zilibuniwa na Mary Quant ambaye ni mbunifu wa mitindo ya nguo kutoka Uingereza. Kwa maneno yake mwenyewe, Mary Quant aliwahi kunukuliwa na gazeti la People Weekly la Uingereza la Aprili 4, 1988 akisema kuwa  lengo lake ni “kuwapatia mavazi wanawake ambayo yatawafanya wanaume wajisikie kuvua nguo mara moja”.

Gazeti la Business Week la Marekani la Juni 8, 1968, lilimnukuu Mary Quant akieleza kuwa alikuwa anabuni mitindo ya nguo ili “kushtua” watu na alieleza kuwa “Kama nguo haziwezi kukufanya uvute watu, basi nadhani kununua nguo hizo ni kupoteza pesa tu”. Alipoulizwa na gazeti la Readers digest la Marekani toleo la Juni, 1967, kwa nini mitindo ya nguo hubuniwa na mitindo hiyo inawapeleka watu wapi, alijibu kwa kifupi kuwa ni “ngono”.

Katika mahojiano mengine na gazeti la News week la Novemba 13, 1967, Mary Quant alieleza kuwa “Je, mimi ni mtu pekee niliyewahi kutamani kwenda kulala na mwanaume wakati wa mchana? Mwanamke yeyote anayeheshimu sheria, kwa mazoea ya zamani, alikuwa anasubiri hadi giza liingie ndipo akalale na mwanaume. Kuna wasichana wengi ambao hawawezi kusubiri hadi giza liingie. Nguo fupi ni kwa ajili ya hao”.

Zaidi ya kubuni mitindo ya nguo, Mary Quant ni mtengenezaji wa vipodozi ambavyo pia vina lengo lile lile kama nguo fupi. Katika mahojiano yake na gazeti la News week, Mary Quant alieleza kuwa “Mapambo yote haya yanawekwa kwenye mwili ili kumshawishi mwanaume alale na mwanamke”.

Maelezo haya ya mbunifu wa mitindo ya mavazi na vipodozi ni sababu tosha kwa wakristo kuzingatia maelekezo ya Mungu kupitia kwa Paulo na Petro juu ya uvaaji wa nguo za heshima.

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mavazi, mapambo na vipodozi?

Basi jipatie kitabu chetu kinachoitwa Mwonekano wa Mkristo: Kanuni Zinazokubalika Kibiblia, Kiafya na Kijamii Kuhusu Mavazi, Mapambo na Vipodozi. Ili kupata kitabu hiki, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail:  spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.

Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mapngo wa Mungu kuhusu mafanikio yako?

Basi jiunge na mtandao wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio. Mtandao huu umeanzishwa kwa kusudi la kuwapatia maarifa ya msingi katika nyanja mbalimbali za maisha. Katika mtandao huu utapata maarifa katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano, malezi ya watoto na mambo mengine ya kiroho kupitia email yako kila zinapowekwa kwenye mtandao huu.

Kujiunga na mtandao huu, jaza fomu hii hapa chini.

About Devotha Shimbe

Devotha Shimbe ni Mwalimu na mwanasaikolojia. Amepata pia mafunzo ya Theolojia. Devotha amejitoa kumtumikia Mungu katika maisha yake yote na amekuwa akifundisha na kutoa semina mbalimbali kuhusu mahusiano na maisha ya kiroho kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *