Rafiki yangu mpendwa katika Kristo
Tafiti zilizofanyika katika nchi mbalimbali duniani zinaonesha kuwa mojawapo ya mambo yanayoongoza kusababisha migogoro na hata kuvunjika kwa ndoa ni fedha. Fedha zinaweza kuchangia migogoro katika ndoa kwa namna nyingi. Namna mojawapo ni kukosa uwazi katika masuala ya fedha baina ya wanandoa. Inasikitisha kwamba, kuna ndoa ambazo, mume na mke hawajui kipato cha mwenzi wake na namna anavyotumia kipato hicho. Katika mazingira hayo, ni rahisi kutokea migogoro baina yao.
Katika makala haya, tutaangalia kwa kifupi namna ambavyo, kukosekana kwa uwazi katika ndoa kunaweza kuvuruga mahusiano katika ndoa ambapo tutaangalia usiri katika matumizi ya fedha na madeni ya siri.
Matumizi ya Siri
Kama wanandoa hawapangi pamoja mapato na matumizi yao, kuna uwezekanao kila mmoja akawa anafanya matumizi bila mwenzake kujua. Hili lisiporekebishwa linaweza kuibua mgogoro.
Wakati mwingine si lazima mwanandoa awe amefanya matumizi mabaya bali ile tu kufanya matumizi kwa siri na mwenzi wako akagundua, tayari ni tatizo ambalo ni ishara ya kutokuaminiana. Kwa mfano, ikiwa mwanandoa mmoja anawasaidia ndugu zake bila kumjulisha mwenzake na ikatokea mwenzako akagundua kunaweza kutokea mgogoro. Au ikiwa mmoja amefungua biashara bila kumshirikisha mwenzake na mwenzi wake akaja kugundua, hapo kunaweza kutokea mgogoro.
Hakuna ubaya kabisa kuwasaidia ndugu wala kuanzisha biashara na huenda kama mtu huyo aliyeyafanya haya angemshirikisha mwenzi wake asingekuwa na tatizo na huenda hata yeye angeweza kumuunga mkono kwa kutoa pesa yake. Changamoto huibuka pale ambapo mwenzi wake amefanya kwa usiri, basi inakuwa tatizo. Hili linaweza kuepukwa tu kwa kuwa na uwazi katika mapato na matumizi ya wanandoa. Njia nzuri na rahisi ya kuwa na uwazi katika mapato na matumizi ni kuwa na bajeti ya familia ambapo mtaainisha mapato yenu yote na mipango ya matumizi kwa pamoja.
Madeni ya Siri
Kama ilivyo kwenye matumizi ya siri, mikopo ya siri nayo inaweza kuleta mgogoro katika ndoa. Mwanandoa mmoja anaweza kuchukua mkopo bila kumshirikisha mwenzi wake na kama baadaye mwenzi wake akigundua kunaweza kutokea mgogoro.
Kuingia kwenye mkopo kwa siri kunaweza kumsababishia mwanandoa huyo kufanya mambo mengine kwa siri. Kwa mfano, ili kulipa mkopo inabidi asiwe muwazi katika matumizi ili apate fedha ya kulipa mkopo kwa siri
Pia, kupata mkopo kunaweza kuwa kunahusisha mambo ya siri kama vile kuchukua nyaraka za familia au za mwenzi wake na kuzitumia katika mkopo. Nyaraka hizo zinaweza kuwa hati za umiliki wa mali kama vile nyumba na kiwanja.
Hebu fikiria, mgogoro unaoweza kuibuka, kama mwanandoa mmoja amechukua mkopo na akashindwa kulipa na alichukua mkopo huo kwa kutumia nyaraka za familia au za mwenzi wake. Hapa lazima mwenzi wake atawajibika katika deni hilo wakati hakuhusishwa. Katika mazingira kama haya, lazima kutokee mgogoro.
Ili kuepusha migogoro ya aina hii, uwazi unahitajika. Kabla ya mwanandoa yeyote kuchukua mkopo amweleze mwenzake hata kama mwenzi wake huyo hatahusika kwa vyovyote na ukopaji wala ulipaji wa mkopo huo. Kwa vyovyote vile, mkopo uliochukuliwa na mwanandoa unamuathiri pia mwenzi wake kwa namna mbalimbali. Kwa sababu hiyo, kuna haja ya kuwa wazi ili kuepusha migogoro.
Kukosekana kwa uwazi kunaweza kusababisha matumizi mabaya ya fedha kama vile kununua vitu visivyo vya lazima na kuacha vitu vya lazima kama vile chakula, mavazi, kulipa ada za watoto na mahitaji mengine muhimu ya familia. Zaidi ya hapo, kukosekana kwa uwazi kunaweza kusababisha tabia zisizo nzuri kama vile uzinzi na ulevi.
Katika njia yoyote ile utakayoamua kusimamia fedha na mwenzi wako, kama wewe ni Mkristo unapaswa uchague njia ambayo itawafanya muwe kitu kimoja badala ya kuwafanya muwe watu wawili.
Wakati Mungu anaanzisha taasisi ya ndoa, alitoa maelekezo mahususi kuhusu uwazi katika ndoa. Hivyo , usiri ni kinyume na kusudi la Mungu wakati anaanzisha taasisi hii nyeti. Mungu ya Mungu yanasema “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja. Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya” (Mwanzo 2:24-25).
Kwa maelekezo hayo ya Mungu, unapokuwa katika mahusiano ya ndoa, kipaumbele chako ni katika mambo yenu (wewe na mwenzi wako) na siyo mambo yako binafsi. Mnapokuwa katika mahusiano ya ndoa mnakuwa timu moja na hivyo mambo yenu yote mnapanga pamoja. Ikiwa kila mmoja anapanga kivyake, mnakuwa pamoja lakini siyo wamoja na hivyo siyo mwili mmoja.
Wanandoa wengi hawana tatizo la uwazi katika masuala ya kimwili, lakini linapokuja suala la fedha, hali inabadilika. Wanandoa wa kwanza duniani, Adamu na Hawa walikuwa uchi na hawakuona haya (Mwanzo 2:25), wanandoa wa leo nao huwa hawaoni haya kuwa uchi. Kama hakuna tatizo kuona uchi wa mwenzi wako, inakuwaje tatizo kujua kipato cha mwenzi wako namna anavyokitumia?
Katika 1 Wakorintho 7:4 Wakristo wanaambiwa kuwa “Mke hana amri juu ya mwili wake bali mumewe, vivyo hivyo mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Uchi wa wanandoa unaotajwa katika Mwanzo 2:25 haupaswi kuishia kwenye uchi wa kimwili tu bali wanapaswa kuwa uchi kwa kila jambo, yaani uwazi katika kila jambo. Wenzi wanapaswa kufahamu kila kitu cha mwenzake yakiwemo masuala ya pesa. Inashangaza kwamba mtu yuko tayari kuwa uchi wa mwili kwa mwezi wake, wakati mwili una thamani kubwa na kuficha fedha ambayo thamani yake ni ndogo kuliko mwili. Thamani ya mwili haiwezi kulinganishwa na fedha hata kama ni nyingi kiasi gani. Hakuna kitu cha thamani kuliko mwili wa mwanadamu.
Ungependa Kujifunza Zaidi Juu ya Mada hii?
Rafiki yangu mpendwa, huenda bado una maswali mengi kuhusu namna unavyoweza kuendesha maisha ya uwazi katika maisha ya ndoa. Usiwe na wasiwasi, tuna kitabu mahususi kuhusu mada hii pamoja na mada zingine kuhusu fedha katika ndoa na familia.
Kitabu hicho kinaitwa Siri za Mafanikio ya kifedha Katika Ndoa na Familia: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi za Kukabiliana na Changamoto na Migogoro ya Kifedha Katika Ndoa na Familia.
Kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu hiki bonyeza hapa
Ili kupata vitabu hivi, wasiliana nasi kupitia namba za simu; +255754-405582 (Simeon Shimbe), +255714-606278 (Devotha Shimbe) na E-mail: spshimbe@gmail.com, devothashimbe@gmail.com.
Je, unataka kupata mafunzo endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?
Kama unataka kuendelea kujifunza kuhusu masuala mbalimbali juu ya mafanikio kwa mkristo unaweza kujiunga na mtandao huu ili uweze kupata makala mbalimbali juu ya masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi. Kwa kufanya hivyo, utapata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.
Ili kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.