Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Mojawapo ya changamoto ambayo inaelekea kuwa janga hapa nchini na duniani kwa ujumla ni omba omba. Ninapozungumzia ombaomba simaanishi wale tu wanaosimama au kutembea mitaani na vibakuli kuomba misaada. Ndiyo, hao ni omba omba, lakini pia wapo omba omba wasiotembea au kusimama mitani lakini wanaomba misaada kwa njia mbalimbali. Baadhi yetu tukikutana na ombaomba huwa tunawapotezea, lakini baadhi yetu huwa tunawapa misaada tukidhani kuwa kufanya hivyo ni kuonesha ukristo kwa vitendo. Kama unadhani kumsaidia kila omba omba ndiyo ukristo, unahitaji kusoma vizuri Biblia yako, ili ujiridhishe kama unachokifanya kinapatana na Biblia.
Ni kweli kwamba ni wajibu wa wakristo kuwasaidia wahitaji katika jamii. Hivyo, zaidi ya kutoa zaka na sadaka kanisani, wakristo yawapasa kutenga kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya kuwasaidia wahitaji. Suala hili ni la kibiblia maana ipo mifano mingi katika maandiko ya watu waliotoa misaada kwa wahitaji.
Mtume Paulo aliwahimiza Waefeso kufanya kazi kwa faida yao na ya wengine (Waefeso 4:28). Licha ya kuhimiza wengine, Paulo alifanya kazi kwa bidii kwa faida yake binafsi na ya wengine. Hii inadhihirika katika hotuba yake kwa wazee wa Efeso kabla ya kusafiri kwenda Mileto ambapo alisema “Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami”(Matendo 20:33, 34).
Mafundisho ya Paulo kwa maneno na vitendo yanaendana na mafundisho ya Yohana mbatizaji ambaye anashauri kwamba matunda ya kazi zetu yawasaidie watu wanaotuzunguka “Akawajibu akiwaambia, Mwenye kanzu mbili na ampe asiye na kanzu; na mwenye vyakula na afanye hivyo” (Luka 3:11).
Ili tuweze kuwasaidia wengine, ni lazima tuwe na kitu cha kuwasaidia. Tunapataje kitu cha kuwasaidia wengine? Ni kwa kufanya kazi. Hapa suala si kufanya kazi tu, bali kufanya kazi kwa bidii ili kupata vitu vya kututosha sisi na kuwasaidia wengine. Kama sisi wenyewe ni ombaomba, tutawezaje kuwasaidia wengine? Mkristo asiyefanya kazi, hawezi kuwa na kitu cha kuwasaidia.
Ukisoma katika Luka 7:2-4, kuna kisa cha akida mmoja ambaye hakuwa Myahudi lakini alionekana wa maana katika jamii kiasi cha wazee wa kiyahudi kwenda kwa Yesu kumuomba aje amponye mtumwa wa huyo akida. Huyu akida alikubalika kutokana na huduma yake ya kuijali jamii kwani aliwajengea sinagogi. Je, wewe ni mmoja wa wakristo ambao kuwepo na kutokuwepo kwao hakuleti tofauti katika familia na jamii yako? Je, familia yako na jamii yako wanafaidikaje na kazi yako?
Katika Matendo 9:36-41, tunakutana na kisa cha Dorkasi. Huyu ni mwanamke aliyekuwa msaada sana katika jamii yake kiasi kwamba jamii ilishindwa kujizuia mara baada ya kufariki kwake. Biblia inaeleza kuwa watu walitumwa kwenda kwa Petro ili aje afanye huduma ya kurudisha uhai wa Dorkasi, yaani amfufue. Kazi ya Dorkasi ilikuwa yenye msaada kiasi cha jamii kuona hastahili kufa. Dorkasi alifanya kazi ya ushonaji nguo, ambazo zilimfanya awe na kitu cha kuisaidia jamii yake. Licha ya kuwasaidia wajane, alitoa sadaka pia kanisani. Hebu kila mmoja wetu ajiulize, hivi nikifa leo, na kuwe na uwezekano wa kufufuliwa lakini kwa sharti kwamba jamii iridhie kufufuliwa kwangu, je, jamii itaridhia nifufuliwe? Mwenzi wangu na familia yangu je, wataridhia?
Pamoja na kwamba ni wajibu wetu kuwasaidia wahitaji, lakini kuna watu ambao ni wahitaji kwa sababu tu hawataki kufanya kazi. Wapo watu wenye uwezo wa kufanya kazi lakini hawataki kufanya kazi au wanafanya kazi kwa uvivu na hivyo wanaishia kuwa wahitaji. Wapo wengine, hasa vijana waliobahatika kusoma, wanasubiri kupata kazi ya kuajiriwa tu na kwa kuwa siku hizi kuna tatizo la ajira, vijana hao wamebaki kuwa omba omba wakati wangeweza kufanya kazi za mikono wakajipatia kipato cha wenyewe.
Watu wote ambao wana uwezo wa kufanya kazi lakini, kwa sababu yoyote ile, hawafanyi kazi, hatuwajibiki kuwapatia mahitaji yao badala yake tunawajibika kuwasaidia wafanye kazi. Utaratibu wa kibiblia wa kuwasaidia wahitaji, unawataka wahitaji wafanye kazi pale inapowezekana. Hakuna nafasi kwa uvivu katika maisha ya mkristo.
Katika Agano la kale, Mungu alitoa maelekezo ya namna ya kuwasaidia wahitaji kupitia kufanya kazi: “Nanyi hapo mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa pembe za shamba lako, wala msiyakusanye masazo ya mavuno yako; utayaacha kwa ajili ya huyo maskini, na mgeni; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu” (Mambo ya Walawi 23:22). Maelekezo haya yanathibitisha juu ya umuhimu wa wahitaji kupata msaada kwa kufanya kazi. Hapa, Mungu hasemi kwamba wavune kila kitu na kisha wawagawie wahitaji bali Mungu anaelekeza kwamba wanapovuna waache sehemu fulani ya mavuno ili wahitaji waje wavune wenyewe. Katika utaratibu huu, hakukuwa na cha bure.
Kwa upande wake, mtume Paulo anaonya vikali juu ya watu wasiopenda kufanya kazi na anatoa maelekezo ya namna ya kushughulika nao: “Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine. Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe” (2 Wathesalonike 3:10-12).
Kwa maelekezo haya machache kutoka katika Biblia, ni dhahiri kuwa si utaratibu wa Mungu kwamba mtu apate mahitaji yake bila kufanya kazi ikiwa uwezo wa kufanya kazi anao. Kwa sababu hiyo, tusivunje utaratibu wa Mungu kwa kutoa misaada kwa watu wasiotaka kufanya kazi. Hata kama ni watoto wetu, tusikubali wale chakula bila kufanya kazi. Tuwape majukumu ya kufanya ili apate haki ya kula chakula. Kwa wale, ambao kwa sababu moja ama nyingine hawana uwezo wa kufanya kazi, hao tunaweza kusaidia bila wao kufanya kazi.
Hivyo, kwa neema yake, Mungu atuwezeshe kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya mahitaji yetu na ya wale wasioweza kufanya kazi huku tukiwasaidia kufanya kazi wahitaji wenye uwezo wa kufanya kazi.
Je, ungependa kujifunza kwa undani juu ya masuala ya fedha kwa mtazamo wa Biblia?
Basi soma katika kitabu kiitwacho:SIRI ZA MAFANIKIO YA KIFEDHA KATIKA NDOA NA FAMILIA: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi na Kukabiliana na Migogoro na Changamoto za Kifedha Katika Ndoa na Familia.
Katika kitabu hiki, utajifunza mambo mengi kuhusu elimu ya fedha kwa muktadha wa kibiblia na namna unavyoweza kuitumia elimu hiyo katika kusimamia fedha zako kama mwanandoa na mwanafamilia,. Ili kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu kitabu bonyeza hapa.
Je, unataka kujifunza zaidi kuhusu mpango wa Mungu kuhusu mafanikio yako?
Unaweza kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio.
Mtandao huu umeanzishwa kwa kusudi la kuwapatia maarifa ya msingi katika nyanja mbalimbali za maisha hususani katika maeneo ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano, malezi ya watoto, ustadi wa kuandaa na kuwasilisha mahubiri na mambo mengine ya kiroho. Kwa kujiunga na mtnadao huu, utaweza kupata makala za mafundisho hayo kupitia email yako kila zinapowekwa kwenye mtandao huu.
Kujiunga na mtandao huu, jaza fomu hii hapa chini.