Hivi Ndivyo Watu Hutajirika kwa Kutumia Ushirikina – 3

Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,

Karibu tena kwenye mfululizo wa makala kuhusu uhusiano wa ushirikina na mafanikio ya kiuchumi. Katika makala yaliyopita tuliona kuwa kuna watu wanadai kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi kwa kutumia ushirikina. Nilieleza hayo kwa kutumia sayansi ya tabia ya mwanadamu. Hata hivyo, ukweli ni kwamba mafanikio hayo hayaletwi na ushirikina bali imani ya mtu husika katika mafanikio.

Kupata makala ya nyuma kuhusu mada hii bonyeza hapa na pia hapa.

Katika makala ya leo, pamoja na mambo menghine, tunaona ni nini watu wanaenda kutafuta utajiri kwa waganga wakati waganga wenyewe wengi wao ni masikini!  Na pia tutaangalia jinsi ambavyo unaweza kutumia mbinu hizi wanazotumia waganga bila ya wewe kuwa mshirikina na ukafikia mafanikio ya aina yoyote unayoyataka.

Waganga wanatumia mbinu gani kuwasaidia watu kupata utajiri?

Watu wanaokwenda kwa waganga ili kupata utajiri au mafanikio mengine hupewa masharti ambayo ni magumu kwa kiasi fulani. Watu hawa huambiwa wakivunja tu masharti hayo, hawawezi kufanikiwa au mafanikio yao yataondoka mara moja. Kama mtu atafanikiwa kwa kufuata masharti haya, anaweza kuamini kwamba ushirikina ndio umemletea mafanikio lakini siyo kweli

Siri iliyoko hapa ni kwamba masharti anayopewa humjengea mtu nidhamu kubwa katika mambo mengi na pia kumfanya aweze kufanya kazi kwa juhudi kubwa kuliko wengine ambao wanafanya anachofanya. Kwa mfano, mganga anamwambia mtu kila siku aamke mapema sana asubuhi kabla watu wengine hawajaamka na apasue nazi kwenye njia panda ndipo aende kwenye shughuli zake.

Kimsingi, hakuna uhusiano wowote kati ya kupasua nazi na mafanikio ya kiuchumi ila kuamka asubuhi na mapema kila siku kunamsaidia kuongeza muda wa kufanya kazi na hivyo kumfanya afanikiwe kuliko wengine.  Kwa kuwa mtu huyu ameaminishwa kuwa asipozingatia masharti haya hawezi kufanikiwa, itabidi ayazingatie kikamilifu hata kama kuna siku hajisikii kufanya hivyo itambidi ajisukume tu kwa hofu ya kuvunja masharti.

Sasa, mtu mwingine ambaye hana  sharti la aina hii, siku akiwa hajisikii vizuri analala, siku nyingine anachelewa na hivyo anashindwa kufikia mafanikio makubwa kwa sababu hafanyi kazi kwa bidii na anapoteza muda mwingi tofauti na mwenye masharti. Masharti mengine kama kutokufanya starehe, kutokunywa pombe, kutokuwa mzinzi, kuvaa nguo moja na mengine mengi yanamfanya mtu kupunguza matumizi na kupata muda mwingi wa kufikiria kazi au biashara yake.

Yapo pia masharti yenye lengo la kumfanya mtu aondoke kwenye woga wake (comfort zone). Kila mmoja wetu ana vitu fulani ambavyo anaogopa kufanya, lakini vitu hivi ndio vinaweza kumletea mafanikio. Ili kumuondoa katika woga huu, mganga anamfanya mtu afanye jambo kubwa ambalo litamuondolea woga kabisa. Kwa mfano, mtu anaambiwa aue, kwa kuona kwamba ameweza kuua mtu, inamfanya asiogope kufanya kitu kingine chochote. Kufanya jambo la kutisha kama kuua hakuleti utajiri kabisa isipokuwa kunamjengea tu mtu ujasiri wa kufanya mambo makubwa bila hofu.

Ubaya wa ujasiri huu ni kwamba unamuondolea mtu hofu ya dhambi. Hivyo, si vema kabisa mkristo anayemcha Mungu kujihusisha na ushirikina maana ushirikina kwa wenyewe tu  ni dhambi lakini pia unakujengea ujasiri wa kutenda dhambi zingine.

Mpendwa msomaji, ni vema ifahamike kuwa masharti unayopewa na mganga hayana chochote cha ajabu bali ni kanuni za kawaida tu zinazotumiwa na watu wengi kufikia mafanikio ila mganga anakufanya uamini kuwa kuna kitu cha ziada nyuma ya masharti hayo.  

Lengo la masharti haya unayopewa na mganga ni kukusaidia kukujengea utaratibu ambao lazima kila siku utaufuata na pia kukujengea nidhamu binafsi ambayo itakusaidia kujisukuma kufanya jambo hata kama hujisikii kufanya. Na hili ndio hitaji kubwa la kuweza kufikia mafanikio. Sasa mtu unapofanikiwa unaamini kuwa ni kuna siri ya mafaniko ambayo mganga anayo inayotokana na nguvu za ushirikina lakini kumbe ungeweza kupata mafanikio hayo kwa kujiwekea masharti wewe mwenyewe ya kukusaidia kujisukuma na kuwa na nidhamu ya mambo fulani bila hata kwenda kwa mganga.

Kwa nini waganga wanatoa masharti kwa wengine lakini wao hawayatumii?

Kipo kitu kimoja cha ajabu ambacho mtu yeyote mwenye akili kitamfumbua macho asiende kabisa kwa waganga kutafuta utajiri na mafanikio mengine. Kitu hicho ni kwamba waganga wengi wanaodaiwa kuwasadia watu kuwa matajiri, wao wenyewe ni maskini wa kutupwa!

Mtu unaweza kujiuliza, kama kweli dawa na masharti ya waganga yanawafanya watu wawe matajiri, kwa nini sasa waganga wenyewe hawayatumii? Ina maana wao hawapendi utajiri? Eti mtu anakupatia dawa ya mafanikio unajenga nyumba wakati yeye anaishi kwenye nyumba ya nyasi! Au anakupatia dawa ya kufaulu darasani wakati yeye hata mtihani wa darasa la nne tu alifeli! Sababu ni moja tu. Pamoja na kwamba waganga wanajua mashari yao yanavyofanya kazi lakini hawana mtu wa kuwajengea imani hiyo kubwa kwao wenyewe.

Mambo yanayohitaji kujisukuma yanahitaji mtu wa kukujengea imani na  kukusaidia kujisukuma ili uyafanye. Pamoja na ukweli huo, si lazima mtu huyo awe mganga wa kienyeji, Unaweza kutafuta mtu yeyote akusaidie kujisukuma. Je, ni mtu gani sahihi wa kukusaidia kujisukuma katika kufanya mambo yako ili hatimaye ufikie mafanikio, Mada hii nitaichambua siku nyingine, Endelea tu kufuatilia.

Kwanini utajiri unaopatikana kwa masharti ya waganga haudumu?

Wengi wa watu wanaopata utajiri kwa masharti ya waganga, hufilisika baadaye kwa sababu wanapopata mafanikio wanasahau kutumia zile kanuni zitokanazo  yale masharti waliyopewa na pia imani yao inakuwa imewekwa kwenye vitu fulani kama vile hirizi badala ya kuwa na imani kwamba wao wenyewe wana uwezo wa kufanikiwa kwa neema ya Mungu na ikiwa tu watazingatia kanuni za mafanikio na kwamba hirizi hazina mchango wowote katika mafanikio yao.

Ufanyeje ili uweze kutumia mbinu hizi kufikia mafanikio?

Unaweza kutumia mbinu za waganga wa kienyeji bila kuvaa hirizi au kupewa masharti na mganga mwenyewe. Cha muhimu hapa ni lazima ujijengee nidhamu binafsi. Yaani, unaweza kujiwekea masharti yako mwenyewe ambayo utayafuata kila siku na uhakikishe unayafuata kweli. Kwa mfano, unaweza kuweka utaratibu kwamba kila siku utakuwa unaamka saa kumi alfajiri na kufanya maombi, kupanga ratiba ya siku yako na kisha kujisomea kidogo. Baada ya hapo unawahi kwenye eneo lako la kazi au biashara na kuanza kazi zako mapema.

Pia unaweza kujiwekea utaratibu kwamba kila mteja au mtu yeyote unayekutana naye kwenye siku husika ni lazima uhakikishe unamfanya ajisikie vizuri kukutana na wewe. Ili kutekeleza sharti hili, utapambana kubuni mbinu za kumfanya kila mtu ajisikie vizuri. Kwa kufanya hivyo, kama wewe ni mfanyabiashara, utakuwa umemvuta kuwa mteja wako wa kudumu. Kama utafuata masharti haya  kila siku, utashangaa kuona mabadiliko makubwa kwenye maisha yako na shughuli zako.

Mpenzi msomaji, unaweza kufanikiwa kwa kiwango kikubwa sana bila ya kutumia ushirikina au kwenda kwa waganga wa kienyeji.

Pamoja na ukweli kwamba ushirikina hauleti mafanikio, kwa nini sasa watu wengi wanaamini kuwa ushirikina unaweza kuwaletea mafanikio. Majibu ya swali hili utayapata katika makala yanayofuata. Endelea kufuatilia……………….

Je, unataka kupata makala endelevu kuhusu mafanikio kwa mkristo?

Basi unaweza kujiunga na mtandao huu ili uwe unapata makala kupitia email yako kila yanapowekwa katika mtandao huu.

Ili kujiunga, jaza fomu iliyoko hapa chini.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *