Unaweza Kuanzia Wapi Katika Safari ya Kujiajiri?
Rafiki yangu Mpendwa,
Karibu tena mpenzi msomaji katika mwendelezo wa waraka kwa wahitimu wa elimu ya juu. Katika sehemu iliyopita ya waraka wangu, nilikuahidi kuwa nitakushauri ni wapi unaweza kuanzia katika safari yako ya kujiajiri baada ya kumaliza masomo yako. Najua kabisa ya kwamba nikikuambia ujiajiri, utanijibu kuwa hauna mtaji. Hata hivyo, uzoefu wangu unaonesha kuwa mtaji ni kichaka tu cha kujifichikia ambacho watu wengi wamekuwa wakikitumia kama sababu ya kutokutaka kuchukua hatua.
Kusoma makala ya nyuma bonyeza hapa
Katika waraka huu, nitapendekeza biashara au shughuli ambazo unaweza kuanza bila kuhitaji mtaji mkubwa na ukaendelea taratibu na kufikia kufanya biashara kubwa. Najua unaweza kunijibu kuwa mtaji huo mdogo utaupata wapi. Jibu langu hapa ni kwamba ukifikiri kwa kina na kuangalia kila kona ya maisha yako hutakosa fedha kidogo za kuanza biashara hizi.
1. Kilimo na ufugaji wa kisasa
Kilimo na ufugaji ni sehemu nzuri sana unayoweza kuanzia kwa mtaji kidogo. Kama unaishi kijijini unaweza kupata eneo zuri ambalo utafanya kilimo au ufugaji wa kisasa. Kwa elimu yako, unaweza kuendelea kujifunza mbinu bora zaidi za kuboresha kilimo au ufugaji wako. Kama upo mjini unaweza kutafuta maeneo ya nje kidogo ya mji na kuanza kufanya shughuli hizi. Japo kilimo kina changamoto nyingi, lakini haimaanishi utashindwa kufanya. Hakuna kitu kisicho na changamoto, hivyo tumia changamoto kama kitu cha kukufanya ufikiri zaidi. Kuna wasomi wenzako wengi tu ambao wamejiajiri katika kilimo na maisha yao yanakwenda vizuri sana.
2. Fanya biashara ya mtandao
Biashara ya mtandao (network marketing) ni biashara ambayo unaweza kuanza na mtaji kidogo na baada ya muda ukatengeneza biashara kubwa sana yenye kipato kikubwa na faida kubwa. Biashara hii inahitaji juhudi zako na kujifunza kwako ili uweze kufanikiwa. Ukifanikiwa, hautakuwa na kikomo cha kiwango cha fedha unachotakiwa kutengeneza na hakuna gharama za kuendesha biashara kulipia kama vile kulipia chumba cha biashara, leseni, kodi za serikali kabla hata hujaanza biashara. Kwa biashara ya mtandao unaweza kufanya biashara kubwa bila ya kuweka gharama zote hizo.
Angalizo ninaloweza kukupa ni kujiepusha na maneno ya watu ya kukatisha tamaa. Badala ya kumsikiliza kila mtu, ni vizuri uonane na watu wanaofanya biashara hiyo ili upate maelezo sahihi au usome vitabu vilivyochambua aina hii ya biashara. Hapo utaweza kutumia usomi wako kufanya maamuzi yako wewe mwenyewe baada ya kupata maelezo sahihi. Kuna wahitimu wengi ambao wanafanya biashara hii na wana mafanikio makubwa.
3. Ujasiriamali wa Taarifa
Katika zama hizi za utandawazi, taarifa zimekuwa ni biashara. Ujasiriamali wa taarifa ni aina ya ujasiriamali ambapo unakuwa unatafuta na kutoa taarifa muhimu ambazo watu wako tayari kulipa fedha ili kuzipata. Biashara hii unaweza kuianza bure kabisa kama tayari una kompyuta yako uliyokuwa unatumia chuoni. Au kama huna unaweza kununua kompyuta ya bei ndogo na kuanza ujasiriamali huu. Unachohitaji kwenye ujasiriamali huu ni wewe kuwa na kiu ya kujifunza na kuwashirikisha wengine taarifa ambazo zitarahisisha au kuboresha maisha yao. Kama taarifa hizo zitaweza kufikia vigezo hivyo watu watakuwa tayari kukulipa ili wapate taarifa zaidi kutoka kwako.
4. Biashara ya uchuuzi
Kama utaona biashara nilizozitaja hazikufai, unaweza kufanya biashara ya uchuuzi. Hii ni biashara ya kununua vitu kwa bei ndogo na kuviuza kwa bei kubwa kidogo ili kupata faida. Angalia ni kitu gani hakipo kwenye eneo unaloishi na angalia jinsi unavyoweza kukipata na kuwapatia kwa bei ambayo wanaweza kumudu na wewe ukapata faida.
5. Endeleza vipaji vyako
Kila mtu ana vipaji vingi ambavyo kama akiweza kuviendeleza anaweza kutengeneza biashara kubwa sana. Vipaji hivyo ni kama vile michezo ya aina mbalimbali, uimbaji, uandishi, uongeaji katika hadhara (public speaking), ubunifu na mengine mengi. Angalia jinsi unavyoweza kutumia vipaji ulivyonavyo kutengeneza kipato na kuweza kujiajiri.
Hii ni baadhi tu ya mifano ya shughuli unazoweza kufanya ili kutengeneza kipato kama hujapata nafasi ya kuajiriwa. Unaweza kufikiria shughuli au biashara zingine zaidi ya hizi. Cha muhimu ni kupenda kile ulichoamua kufanya na kuweka juhudi, ubunifu na maarifa. Inaweza kukuchukua muda kupata matunda lakini unaweza kuja kufurahi baadaye na ukaona tofauti kuwa ya maisha yako na ya wenzako ambao wameajiriwa.
Hapa ndiyo mwisho wa waraka huu mrefu. Ukiwa unahitaji ufafanuzi zaidi au ushauri kuhusu kitu chochote ililichomo katika waraka huu, usisite kuwasiliana nami.
Endelea kufuatilia mtandao huu kwa elimu zaidi kuhusu mafanikio katika nyanja mbalimbali. Ili usipitwe na makala, jiunge na mtandao huu ili uwe kupata makala kupitia email yako kila zinapowekwa katika mtandao huu.
Kujiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini.