Rafiki yangu mpendwa katika Kristo,
Karibu tena katika mwendelezo wa makala juu ya nini husababisha baadhi ya watu wanaopata fedha nyingi kuishia kuwa maskini wa kutupwa. Tayari tulishangalia makundi ya watu wanaopata fedha nyingi na makundi gani yenye uwezekano mkubwa wa kuishiwa fedha na kuwa maskini na nini kinapelekea hali hiyo.
Kabla ya kuendelea na makala ya leo, nakushauri usome makala ya nyuma ili uweze kuwa wa mtiririko kamili wa makala haya.
Kusoma makala ya nyuma kuhusu mada hii bonyeza hapa.
Katika makala ya leo, tutaangalia mambo unayoweza kufanya ili ikitokea unapata fedha nyingi ziweze kudumu na kukufanya uwe na mafanikio endelevu ya kifedha. Mambo hayo ni kama ifuatavyo:
- Jipatie elimu sahihi kuhusu fedha
Fedha ni kitu muhimu sana katika maisha ya mwanadamu yeyote. Kwa sababu hiyo, wanadamu wanapaswa kuwa na elimu sahihi kuhusu fedha ili waweze kuitafuta, kuitumia na kuiongeza kwa namna iliyo sahihi. Kukosekana kwa elimu hiyo, ni sababu inayowafanya watu wapoteze fedha na kuwa maskini hata kama wanazo nyingi.
Pamoja na umuhimu huu, elimu ya fedha haifundishwi ipasavyo na kwa usahihi shuleni, nyumbani na hata kanisani kwa na kwa sababu hiyo kuna watu wengi sana walio na elimu kubwa lakini hawana elimu ya fedha. Hali hii imesababisha hali mbaya ya kifedha kwa watu wengi wakiwemo wasomi. Nakushauri usiwe mmoja wao.
Unaweza kupata elimu ya fedha kwa kusoma vitabu vizuri kuhusu elimu ya fedha, kuhudhuria semina au mafunzo, kupata elimu ya fedha kupitia mtandao na kadhalika.
2. Ikitokea Umepata Fedha Nyingi Kwa Mpigo, Tulizana Kwanza
Kama tulivyoona katika makala ya nyuma, baadhi ya watu wanapopata fedha nyingi kwa mpigo, hufanya vituko vingi katika matumizi ya fedha hizo. Kinachosababisha wafanye hivyo ni kwa sababu hawajipi muda wa kujipanga ni namna gani wataitumia fedha hiyo kwa manufaa ikiwa pamoja na kuizalisha.
Watu wengi wanapopata fedha nyingi hupata msukumo wa kuitumia,hasa katika mambo ambayo hapo awali walitamani kuyafanya lakini hawakuyafanya kwa sababu ya kutokuwa na fedha ya kutosha. Matokeo yake hujikuta wanapigwa na kitu kizito.
Ili kuepuka hali hiyo, unapopata fedha nyingi kama vile fedha ya urithi, mafao ya kustaafu, mauzo ya madini na kadhalika ni vema ukatulizana kwanza na kujipanga vizuri namna utakavyoitumia. Usiwe na haraka kabisa.
Usianze kutumia fedha bila kujipanga vizuri kwa kuwa fedha ambayo haijapangiwa matumizi huwa haikosi matumizi. Yaani, fedha usipoipangia matumizi utajikuta unaitumia katika matumizi ya ovyo. Pale itakapohitajika ni vizuri kupata ushauri kwa watu unaowaamini. Kwa mfano, kama unataka kuwekeza, ni vizuri ukawatafuta watu wenye uzoefu au elimu katika kile unachotaka kuwekeza kuliko kuingia kichwa kichwa.
3. Matumizi Yako Yasizidi Mapato
Kama tulivyoona katika makala ya nyumba, sababu mojawapo inayowafanya watu wanaopata fedha nyingi kuishia kuwa maskini ni dhana kwamba fedha nyingi ndiyo utajiri. Dhana hii si sahihi. Siri kubwa ya utajiri siyo ukubwa wa kipato cha mtu bali ni nidhamu ya matumizi ambapo mapato lazima yawe makubwa kuliko matumizi.
Mapato yanapokuwa makubwa kuliko matumizi unabakiwa na fedha kwa ajili ya kuwekeza kwa ajili ya kupata kipato zaidi na hivyo kupata utajiri na uhuru wa kifedha. Hivyo, unapoipangia matumizi fedha yako hakikisha kuwa matumizi hayo ni madogo kuliko fedha hiyo na fedha inayozidi kwenye matumizi izalishe kwa kufanya biashara au uwekezaji.
Ili uweze kuwa kipato endelevu, hakikisha fedha unayopata unaizalisha na matumizi yako wewe yawe ni ile faida iliyozalishwa na fedha yako, na tena siyo yote kwa sababu unahitaji kuongeza uzalishaji zaidi kutokana na kile ulichozalisha. Nikitumia lugha ya uzalishaji kwa wanadamu na wanyama, edha yako inapaswa izae watoto na hao watoto wazae wajukuu.
Kwa vyovyote vile, usiwe na matumizi yanayozidi kipato chako. Kama unataka kuongeza matumizi, ongeza kwanza kipato. Hakuna muujiza hapa. Ukifuata kanuni hii, utafanikiwa, usipoifuata, usitafute mchawi.
4. Kuwa Makini Na Ndugu, Jamaa Na Marafiki
Nilieleza katika makala ya nyuma, lakini naomba nirudie tena leo. Fedha huwa zinavuta watu, ambao wanaweza kuwa wazuri au wabaya. Kwa bahati mbaya, fedha huvuta watu wabaya zaidi kuliko wazuri.
Watu wakijua una fedha, wanakuwa karibu na wewe si lengo jingine bali ili wanufainike na fedha zako. Unahitaji kuwa makini sana na watu wote wanaokuzunguka, bila kujali unawaamini kiasi gani au mko karibu nao kiasi gani. Usiogope kusema HAPANA pale wanapokuomba fedha kwa ajili ya matumizi ambayo si ya msingi. Wasaidie kwa mahitaji yale ambayo ni ya msingi kweli kama vile matibabu.
Usiogope kuambiwa una roho mbaya. Ni heri wakuone una roho mbaya kuliko uishie kuwa maskini na baadaye ushindwe kuwasaidia hata kwa mahitaji yao ya msingi. Jenga utajiri wako kwanza ili upate uwezo wa kuwasaidia wengi zaidi kuliko kukazana kumsaidia kila mtu wakati hujjenga utajiri wa kutosha na kuishia kuwa maskini. Saidia watu kwa mahesabu na uwe makini na kila ushauri mwanaokupatia kuhusu matumizi ya fedha zako au uwekezaji.
5. Kuwa na Mtazamo Mpana na Fedha Katika Akili Yako
Mtazamo wako kiakili kuhusu fedha ni muhimu sana katika mafanikio ya kifedha. Kama mtazamo wako wa sasa ni shilingi milioni moja, basi panua mtazamo huo na kuwa milioni mia au zaidi. Yaani kama kwa sasa, unawaza kuwa kipato cha shilingi miliono moja kinakutosha kuendesha maisha, panua mawazo hayo yawe milioni mia au zaidi na uiwekee mipango hiyo fedha. Hii itakusaidia ukipata fedha nyingi kwa mkupuo hutafanya vituko bali itakukuta umejiandaa kiakili kuwa nayo.
Ili kuweka katika vitendo hiki ninachokushauri, fanya hivi: Uwe na daftari la malengo na mipango na katika daftari hilo andika “nikiwa na milioni……(andika kiwango cha fedha) nitafanya yafuatayo…….”(orodhesha mambo hayo unayopanga kufanya ikiwa utapata kiasi hicho cha fedha ulichokitaj). Fanya zoezi hili mara kwa mara na kwa kufanya hivyo utaanza kujizoesha viwango vikubwa vya fedha na hivyo utakapozipata hutababaika kama ambaye hana mpango kama huo.
Rafiki yangu mpendwa, bila shaka haya machache yamekupatia mwanga juu ya namna unavyoweza kunufaika na fedha nyingi kama utazipata badala ya kuwa kama wale wanaopata fedha nyingi leo na kesho ni maskini wa kutupwa. Nikutakie kila la heri.
Je, Unataka Kupata Mafunzo Endelevu Kuhusu Mafanikio?
Kwa kuwa tumeona kuwa kuna umuhimu wa kupata elimu sahihi ya fedha ili uweze kupata mafanikio ya kifedha, karibu upate kitabu kizuri kuhusu: SIRI ZA MAFANIKIO YA KIFEDHA KATIKA NDOA NA FAMILIA: Kanuni za Kibiblia na Kiuchumi za Kukabiliana na Migogoro na Changamoto za Kifedha Katika Ndoa na Familia.
Ili kupata maelezo zaidi kuhusu kitabu hiki bonyeza hapa.
Zaidi ya kuwa na kitabu hiki, unaweza kupata elimu endelevu kuhusu masuala ya fedha na mengineyo kwa kujiunga na mtandao huu wa Mkristo na Maisha ya Mafanikio.
Kupitia mtandao huu utaweza kupata makala mbalimbali kuhusu masuala ya fedha, biashara, uwekezaji, mahusiano (uchumba na ndoa), maisha ya kikristo, malezi ya watoto na mengine mengi.
Kama utajiunga na matandao huu, utaweza kupata makala kupitia email yako moja kwa moja kila zinapowekwa katika mtandao huu.
Ili kujiunga jaza fomu iliyoko hapa chini.
Hapa umeuliza swali au umetoa maoni?