Epuka Tabia Hizi Mbaya Unapokuwa Katika Mazungumzo – 2

Rafiki yangu mpendwa,

Karibu katika mwendelezo wa makala kuhusu tabia mbaya unazopaswa kuziepuka unapokuwa katika mazungumzo muhimu na mtu. Katika makala yaliyopita, tuliangalia tabia mbili ambazo zinaweza kuharibu mazungumzo yako na mtu au watu wengine. Tabia ya kwanza ni kumkatiza mtu mwingine anapoongea na tabia ya pili ni kumalizia maneno au sentensi za mtu mwingine.

Kusoma makala ya nyuma bonyeza hapa

Leo tutaangalia tabia mbaya zingine tano. Tabia ya kwanza ni matumizi ya simu wakati wa mazungumzo. Tabia ya pili ni kejeli, utani na ubishi na ya tatu ni kutokumtazama mtu unayeongea naye. Tabia ya nne ni kukosa utulivu na ya tano ni kuonesha kujua kila kitu.

Matumizi ya Simu wakati wa Mazungumzo

Si ustaarabu hata kidogo kuendelea kutumia, simu iwe kupokea, kupiga au kutuma ujumbe mfupi wa maneno, ukiwa katikati ya mazungumzo na mtu. Bila kumung’unya maneno, hii  ni dharau kubwa.

Wakati pekee ambapo inaweza kukubalika kutumia simu ni pale ambapo unahitaji kumuonesha mtu unayeongea naye kitu fulani kwenye simu yako, kama vile picha. Na hata wakati unapotafuta kitu hicho kwenye simu, unapaswa kumhakikishia mtu huyo kwamba bado unasikiliza kile kinachosemwa. Kwa mfano, unaweza ukawa unatikisa kichwa kuashiria kuwa unasikiliza au unaweza kuwa unamtazama mara kwa mara badala ya kuinama kwenye simu moja kwa moja.

Kama utaendelea kutumia simu wakati mtu mwingine anaongea, ni ishara kwamba hujali kabisa anachoongea kwa sababu kwa vyovyote vile usikivu wako hauwezi kuwa mzuri wakati mawazo yako yamezama kwenye kitu kingine kwenye simu. 

Iwapo una simu muhimu au ya dharura ya kupiga, kupokea au kutuma ujumbe, ni ustaarabu kumuomba ruhusa mtu unayeongea naye. Unaweza kumwambia , samahani sana, naomba nipokee simu hii ni ya muhimu sana au samahani naomba dakika mbili nitume ujumbe mfupi wa simu au nipige simu muhimu kisha tuendelee na mazungumzo yetu. Kwa kufanya hivyo, mtu unayeongea naye ataona umeyapa uzito sana mazungumzo yenu kiasi kwamba hutaki kugawanya usikivu wako. Hata hivyo, si vema kufanya hivyo mara nyingi sana. Fanya hivyo, pale tu ambapo ni muhimu sana kukatiza mazungumzo ili utumie simu.

Kejeli, utani na ubishi

Ikiwa una mazoea ya kutoa matamshi ya kejeli, ubishi na utani katika mazungumzo, inaweza kuleta shida kwa unayezungumza naye. Vyovyote itakavyokuwa, hii inaweza kuonesha kuwa wewe ni jeuri na hauna heshima kwa unayezungumza naye. Kwa sababu hiyo, mtu huyo anaweza kuamua kuachana na mazungumzo yenu au kulazimika kuanza  kujitetea au kutoa maelezo yasiyo ya lazima. Wakati mtu anazungumza na wewe na unatikisa kichwa kukataa anachokieleza au unatoa maneno ya kejeli, inaweza kuashiria kuwa kile anachokuambia ni uongo au siyo sahihi.

Unapoonesha mashaka kwenye kile anachokueleza, itamfanya aonekane mjinga na asiye  na akili. Unapocheka wakati mtu unayeongea naye hajasema kitu chochote cha kuchekesha ni ishara ya dhihaka kwake au hauchukulii uzito kile anachoongea na unaweza kuonekana kuwa mkorofi na usiye na heshima.

Epuka utani mwingi wakati wa mazungumzo muhimu. Utani kwa wenyewe sio lazima kiwe kitu kibaya. Utani unaweza kuwa kilainishi cha mazungumzo na kuyafanya kuwa ya kufurahisha. Hata hivyo, utani uliopitiliza haufai wakati wa mazungumzo muhimu. Vilevile, kuwa mbishi sana kunaweza kuonekana kuwa mtu asiye na adabu, hasa ikiwa unazungumza na mtu ambaye hamjazoeana. Hivyo, pima ni nani unayezungumza naye na uangalie kama ubishi wako au  utani  wako havitaeleweka vibaya kwa mtu huyo.

Ikiwa mtu unayeongea naye atakueleza kitu ambacho si sahihi kwa mtazamo au uelewa wako, ni vizuri ukamuonesha hivyo kwa heshima, tena baada ya kuwa amemaliza kuongea badala ya kuanza kumkatiza kwa kutikisa kichwa, kutoa maneno ya kejeli au kubishana naye bila ustaarabu

Kutokumwangalia Mtu Unayezungumza naye

Mtazamo mzuri wa macho wakati wa mazungumzo ni muhimu Mtazamo wa macho unakuleta karibu zaidi na mtu kuliko maneno. Kutazamana kwa macho kunaweza kuonesha huruma, kuelewa na kujali. Kutazama macho ni aina ya ustadi katika mazungumzo ya ana kwa ana.

Siyo lazima umkodolee macho muda wote mtu unayeongea naye, lakini ni muhimu muda mwingi mkutanishe macho. Usipofanya hivyo, unatoa ishara kwamba hupendezwi au hujavutiwa na kile anachokueleza. Hii inaweza kumkatisha tamaa. Haijalishi ni kiasi gani unatikisa kichwa  kwa nguvu na kuthibitisha ndiyo, niko pamoja nawe, bado mtu anaweza asikuamini kwa sababu macho yako yanasema jambo lingine.

Hebu fikiria, kwa mfano, umeingia dukani, unamsalimia muuzaji na kumuomba bidhaa fulani unayoihitaji. Mtu huyo anaitikia salamu bila kukutazama na kisha anakuonesha kitu hicho huku amekupa kisogo bila kukutazama! Utajisikiaje? Bila shaka, utajisikia kupuuzwa na unaweza usinunue kitu hicho na kuamua kukitafuta katika duka jingine. Hivyo, ndivyo, inavyoweza kutokea kama unaongea na mtu lakini hakuangalii kabisa. Kuangalia kwingine wakati mtu anazungumza nawe ni kukosa adabu. Macho huwa hayadanganyi kamwe. Kumtazama mtu kwa macho kunamaanisha kuwa unamwona na kukiri uwepo wake. Kinyume chake ni kutokutambua na kutokukiri uwepo wake.

Kukosa utulivu wa mwili wako

Tabia nyingine mbaya ni kukosa utulivu wa kimwili wakati wa mazungumzo. Kwa mfano, kuinuka  mara kwa mara na kutembea tembea, kuongea huku unafanya kazi fulani ambayo siyo ya lazima wala muhimu. Vitendo hivi vinaweza kukatisha katisha mazungumzo yenu na vinaonesha kuwa hujali au huthamini mazungumzo yenu.

Kwa kadri inavyowezekana, jaribu kuonesha utulivu na  kujali mazungumzo yenu. Achana na shughuli zingine zisizo muhimu na zisizohusiana na mazungumzo yenu ili kutoonekana kuwa umepuuza mazungumzo na hauna heshima dhidi ya mtu mnayezungumza naye.

Kuonesha kuwa unajua kila kitu

Kujionesha kuwa unajua kila kitu ambacho mtu anazungumza ni tabia nyingine isiyopendeza. Fikiria, unaongea na mtu lakini unakutana na majibu kama vile, hiyo naijua, nilisoma hiyo jana kwenye mtandao, alishaniambia, hilo suala haliko hivyo, hapo unapotosha maana ukweli najua n.k. Bila shaka hutaona sababu ya kuendela kuongea na mtu wa aina hiyo maana kila unachoongea anakijua!

Aina hii ya utukufu humfanya mzungumzaji mwingine aonekane hana akili na asiyejua kitu. Unapodai kujua yote wakati wa mazungumzo, haiwafanyi watu wakuone ni mjuzi wa mambo. Badala yake, inawafanya wakuone kama mtu mwenye kujisikia na asiyeweza kufundishika. Na hii ni tabia ambayo itakuwafanya watu waepuke kuzungumza na wewe.

Hata kama wewe ni ensaiklopidia unayejua kila kitu unachohitaji kujua, ni vizuri uwape watu nafasi ya kueleza mawazo yao. Kiuhalisia, hakuna mtu anayejua kila kitu.  Daima kuna kitu kipya cha kujifunza. Mtu anapokuambia jambo na ukaendelea kusema unajua, unaweza kuwa unajinyima fursa ya kujifunza kitu kipya. Kuwa na mazungumzo na mtu anayejua yote ni kero. Acha kukera watu.

Kwa leo tuishie hapa. Karibu katika mwendelezo wa makala haya.

Endelea kufuatilia makala zaidi katika mtandao huu kwa ajili ya mafanikio yako katika nyanja mbalimbali za maisha.

Kama hujajiunga na mtandao huu, jaza fomu iliyoko hapa chini ili uweze kupokea makala kwenye barua pepe yako moja kwa moja.

About Simeon Shimbe

Simeon Shimbe ni mchumi kitaaluma, mwandishi wa vitabu na makala na mjasiriamali. Amekuwa akiandika kuhusu masuala ya fedha, biashara na uwekezaji na masuala mbalimbali ya kiroho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *